//Siku ya Kiswahili Duniani – 7/7/2023

Siku ya Kiswahili Duniani – 7/7/2023

Waziri, katika Wizara ya Utalii, Wanyamapori na Turathi, Mhe. Peninah Malonza, leo hii amejumuika na wakaazi wa Mombasa ili kuadhimisha Siku ya Kiswahili duniani.

Maadhimisho hayo yalianza na msafara ulioanzia Mapemebeni, na kuelekea hadi kituo cha Utamaduni wa Waswahili, pembezoni Ngomeni.

Novemba 23, 2021, Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO), liliteua Julai 7 kuwa siku rasmi ya kuadhimisha lugha ya Kiswahili duniani, hivyo basi, kuzifanya sherehe hizo kua za pili tangu uteuzi huo.

“Ni jambo la kihistoria kuwa Kiswahili ndiyo lugha pekee ya Kiafrika kutambuliwa na Umoja wa Mataifa. Kwa hivyo ni jukumu letu kuhakikisha kwamba kinazungumzwa na wengi, na kulindwa,” alisema Mhe. Malonza.

Waziri huyo pia aliongezea kwa kusema kua, serikali ya Kenya imeweka mikakati kabambe ili kuikuza lugha ya Kiswahili.

Ningependelea kuwajuza kwamba, Wizara yangu imeanza kuweka mikakati kabambe ya kuunda Baraza Kuu la Lugha ya Kiswahili nchini (National Kiswahili Council) kwa minajili ya kukuza ukuwaji na utumizi wa lugha hii.” Aliongeza Malonza.

Kiswahili ni lugha ambayo iko na takriban wazungumzaji zaidi ya milioni mia mbili, na inazungumzwa na watu wengi Afrika Mashariki.

Sherehe hiyo haitafikia kikomo leo, bali itaendelea kwa muda wa siku tatu mtawaliwa na kufikia tamati hapo Jumapili, tarehe 9 Julai.

Katika sherehe za mwaka huu, watu wataweza kujihusisha na shughuli mbalimbali zikiwemo; maonyesho ya kitamaduni, mihadhara, ukariri wa mashairi, kucheza nyimbo za Taarab, maonyesho ya Mbeja, mazungumzo ya wanawake, zamuni, na mengine mengi.

Katika sherehe hizo, Waziri Malonza alijumuika na Gavana wa Mombasa, Mhe. Abdulswamad Shariff Nassir, Katibu Mkuu katika Idara ya Utamaduni na Turathi za Kenya, Bi. Ummi Bashir, Seneta Miraj Abdillah, Wakurugenzi Wakuu na Wenyekiti wa Mashirika ya Kiserikali, pamoja na viongozi wengine.

By | 2023-07-11T09:34:41+00:00 July 11th, 2023|News&events|0 Comments

About the Author:

Leave A Comment

Skip to content